MADA UWANA WA YESU KRISTO KWA MWENYEZI MUNGU. Kwanza ina tubidi tuweze kuelewa kwamba Mwenyezi Mungu Ana wana wengi tu maana wote waliompokea Aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu wale ambao waliaminilo jina lake kama vile tunavyosoma katika Yohana 1:12,13. Lakini inatupasa kuelewa kwamba licha ya Mungu kuwa na wana wengi anaye mwana wa kipekee ambaye kwake tunapata wokovu wetu. Lakini hebu tuangalie ni kwa nini? Warumi 3:23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; kwa hivyo tunaona kwamba watu wote wametenda dhambi. Sasa je! Yesu Kristo vipi hali yake? 1 Yohana 3: 9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Je! Yesu kristo Alitenda dhambi? 1 Petro 2: 21 Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. 22 Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yohana 8: 46 Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? Kwa hivyo tunaona kwamba Yesu Kristo hana dhambi. Ni kwa nini hakutenda dhambi? Wakolosai 2: 9 Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Sasa tuangalie swala hili kwa ujumla, 1 Yohana 4: 14 Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. 15 Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Ni kwa nini Mungu Akae ndani yake? 1Yohana 5: 1 Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye. Kwa hivyo inatuonyesha kwamba ukimpenda Mwenyezi Mungu utampenda Naye huyo Aliyezaliwa na Mungu. Kwani Mungu Huzaa kivipi? Yakobo 1: 18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake. Kumbe Mungu Huzaa kwa Neno lake la kweli. Hilo pia linadhibitishwa na Quran 3:39…Mara malaika wakamlingania, hali amesimama akisali chumbani, kwamba Mwenyezi Mungu Anakupa khabari njema za kuwa utazaa mtoto umwite Yahya atakayekuwa mwenye kumsadikisha Mtume atakayezaliwa kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu Naye ni Nabii Isa na atakayekuwa bwana kabisa na mtawa na Nabii anayetokana na watu wema. Sasa ukisha kubali kuwa Yesu Kristo Amezaliwa na Mungu basi utakuwa ni mwenye kuushinda ulimwengu…1 Yohan 5: 5 Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Kwani ? utakuwa na ushuhuda wa kweli…1 Yohana 5: 10 Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Kumbe Mwenyezi Mungu Amemshuhudia ! Mathayo 3: 16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; 17 na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Kwa hivyo kama Mungu Amemshuhudia Alikuwa Akituonyesha nini? 1 Yohana 5: 12 Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. 13 Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu. Sasa Qurani nayo inatufundisha nini kuhusiana na swala hili? Muhammad mwenyewe alifahamu jambo moja na akaliona kuwa hatari kubwa haswa kwa wafuasi wake ambao wanamuamini sana. Alijua tu kwamba akisema kuwa Mwenyezi Mungu Ana Mwana basi watu wote wangelimuami huyo mtoto na kupata uzima wa milele na ndio akasema katika Qurani 43:81..sema, Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema angalikuwa na mtoto ningekuwa wa kwanza wa kumuabudu mtoto huyo kwa kuwa ni mtoto wa Mola wangu. Hili linaonyesha kwamba alikuwa ametambua maneno Aliyoyasema Yesu kristo katika Yohana 5: 20 Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu. 21 Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao. 22 Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; 23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Kwa hivyo alijua tu itambidi amueshimu Yesu Kristo kama anavyo mheshimu Baba kwa kila jambo na ndio akasema Mungu hakuzaa wala hakuzaliwa Qurani 112:3. Lakini hebu tudondoe tena kidogo. Qurani 4:136 inasema; kwa kunukuu tu,…anayemkanusha Mwenyezi Mungu, na malaika zake, na mitume wake, na vitabu alivyoteremsha…siku ya kiyama atakuwa katika upotevu ulio mbali kabisa. Swali la kujiuliza, Mungu Amesema nini kuhusiana na Yesu Kristo kuwa mwanawe? Tusome Mathayo 17: 5 Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Tunaona hapa Mungu Anashuhudia kuwa Yesu Kristo ni mwanawe na hilo halipingiki maana Mungu haulizwi maswali. Soma Qurani 21:23. Je! Sauti hiyo ilishuhudiwa? Ndio, ilishuhudiwa na wanafunzi wa Yesu Kristo maana walikuwa pamoja naye hapo mlimani. 2 Petro 1: 17 Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. 18 Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Malaika naye alisema nini? Soma luka 1: 35 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Hapa tunaona malaika anashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Pia ukisoma Qurani 19:19 utaona Yesu Kristo anaitwa na malaika Jibril Mwana Mtakatifu. Mitume walisema nini? Soma mathayo 16: 13 Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? 14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. 15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? 16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. 17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Wanafunzi wa Yesu wenyewe wanashuhudia kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Je! Yesu Kristo anashuhudia yeye ni Mwana wa nani? Yohana 10: 36 je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? Kumbe Alikuwa amesema hapo mwanzoni katika hio hio Yohana 9: 35 Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? 36 Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? 37 Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye. Hapa tunaona Yesu Kristo mwenyewe akishuhudia kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Sasa kuna faida gani ya kumtambua huyu Hapa tunaona Yesu Kristo mwenyewe akishuhudia kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Sasa kuna faida gani ya kumtambua huyu Yesu Kristo? Tunaposoma Yohana 3: 36 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia. Sasa kuepkana na gadhabu ya Mungu tufanye nini? Basi tukisha mwamini tutahitaji kubatizwa ubatizo aliobatizwa. Mathayo 3: 13 Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. 14 Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? 15 Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. 16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; 17 na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Basi sasa fanya uamuzi ulio bora kumfwata Mwana wa Mungu kama yule towashi katika Matendo ya mitume 8: 36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? 37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu. 38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. 39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. Kwa hivyo ni vyema uweze kumkubali Mwana wa Mungu ili upate uzima wa milele katika jina la mwana wake Yesu Kristo. Amina na Bwana Akubariki.
welcome and lets study together
— Admin, 06 Apr 2026 07:36